Aina Mpya za Mbegu za Mazao
Kamati ya Taifa ya Mbegu ( National Seed Committee ) imeidhinisha matumizi ya aina 29 za mbegu mpya za mazao mbali mbali ya kilimo. Mazao hayo ni mahindi, mpunga, alizeti, karanga na chai. Hatua hiyo ya Kamati inalenga kuongeza tija na kipato kwa mkulima. Kuidhinishwa kwa aina hizo za mbegu kunafuatia mapendekezo yaliyofanywa na Kamati ya Taifa ya Kupitisha Aina Mpya za Mbegu za Mazao ( The National Variety Release Committee ) katika kikao chake kilichofanyika makao makuu ya Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dar-es-saalam tarehe 16 na 17 Machi 2016. Aina hizo mpya za mbegu zimepitishwa baada ya kufanyiwa utafiti na kugundulika kuwa zina sifa mbalimbali kama vile kutoa mavuno mengi, kustahimili ukame, ukinzani dhidi ya magonjwa na wadudu, kukomaa mapema na kupendwa na wakulima. Kati ya aina hizo mpya za mbegu, kuna aina 16 za mahindi, 2 za mpunga, 4 za alizeti, karanga 3 na 4 za chai. Mbegu hizo zimefanyiwa utafiti wa kina na vituo vya utafiti vya Umma na sekta binafsi hapa nchini kama...